Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 28 Desemba, 2017 amekutana
kwa mara ya kwanza na kamati maalum aliyoiunda kwa lengo la kuhakiki
mali za chama hicho, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Kamati hiyo aliitangazwa tarehe 20 Desemba, 2017 Mkoani Dodoma na inaongozwa na Dkt. Bashir Ally.
Katika
Mazungumzo hayo Mhe. Rais Magufuli amewataka wajumbe wa kamati hiyo
kufuatilia na kuhakiki mali zote za chama, kumhoji mtu yeyote ambaye
atahitajika kutoa taarifa juu mali za chama na kubaini thamani ya mali,
mahali zilipo, makusanyo ya mapato na wanaozishikilia ama kutumia mali
hizo.
Mhe.
Rais Magufuli pia ametoa wito kwa wanachama wa CCM na wananchi wengine
kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zote zinazohusu mali za chama kwa
kamati hiyo, na watakaoitwa kuhojiwa waitikie wito huo.
“Nataka
mali za chama zikinufaishe chama, nataka mkamhoji mtu yeyote, awe
kiongozi, awe mwanachama, awe mfanyabiashara, mtu yeyote. Mkazihakiki
mali zote ili chama kipate haki yake” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Akizungumza
kwa niaba ya kamati hiyo, Dkt. Bashiru Ally amesema kamati imeanza kazi
rasmi na ametoa wito kwa wanachama, wananchi na wote wanaozitumia mali
za chama kutoa ushirikiano watakapoitwa kuhojiwa.
“Tumezungumza
na Mwenyekiti kwa karibu saa mbili, katueleza matarajio yake, sababu za
kuunda tume hii, kazi zake na faida zake kwa chama na kwa nchi, kwa
hiyo ametukabidhi vitendea kazi na taarifa mbalimbali na ametueleza kazi
yetu ni kuhakiki mali zote za chama kwa kushirikiana na wanachama na
wale wanaoshirikiana na chama kuzitumia hizo mali kama vile wapangaji,
wasimamizi, nakadhalika” amesema Dkt. Bashiru Ally.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
28 Desemba, 2017
No comments:
Post a Comment