Pages

Saturday, January 20, 2018

HUYU NDIYE KOCHA MPYA MFARANSA WA SIMBA ALIYECHUKUA NAFASI YA OMOG…




BAADA ya hadithi za takribani wiki mbili hatimaye Kocha Mfaransa ambaye alikuwa akisubiriwa kutua nchini kuinoa Klabu ya Simba amewasili.

Kocha Pierre Lechantre anayetimiza miaka 68 wiki mbili zijazo, yaani Februari 2, ametua nchini kumalizana na uongozi wa juu wa Simba kabla ya kuanza kazi mara moja.

Lechantre ataanza kazi baada ya kumalizana na Simba zoezi ambalo lilipangwa kufanyika jana na baada ya hapo, leo mara moja, Simba wataanza kushughulikia vibali vyake kwa ajili ya kuhakikisha anaanza kazi.

Kocha huyo Mfaransa alikuwa ni siri kubwa kwa uongozi wa Simba ambao haukukubali kabisa ajulikane wala ahojiwe na waandishi wa habari hadi gazeti namba moja la michezo nchini la Championi lilipomfichua kwa mara ya kwanza jana hali iliyoilazimisha Simba “kushusha silaha chini” na kutoa taarifa kwa vyombo vya habari.

Baada ya kutua nchini juzi usiku, Simba walimficha kocha huyo katika hoteli moja katikati ya jiji. Hoteli ambayo Yanga waliwahi kumficha Kocha George Lwandamina alipotua nchini mara ya kwanza na kuwaficha waandishi, lakini  ikamvumbua Mzambia huyo na kufanya naye mahojiano ya ana kwa ana.

Jana, mambo yalikwenda hivyo hivyo kwa Lechantre ambaye amekutana kwa mara ya kwanza na timu ya waandishi wa SALEHJEMBE ambao walizungumza naye na kupiga naye picha kwa pozi huku wakimsikiliza na kumhoji alichokuwa anakiona.

Hakukuwa na nafasi kubwa ya kumhoji kwa kuwa Simba walishaona “imeshakuwa soo” na kuamua kumhamisha kocha huyo hotelini hapo, ingawa ilielezwa baadaye wangeenda naye Uwanja wa Taifa akaishuhudie Simba ikiivaana na Singida United katika mechi ya Ligi Kuu Bara.

Wakati blogu hii ikifanya maajabu mengine ya kumfichua kocha aliyekuwa amefichwa na waandishi wengine wote kumkosa, Lechantre ni kocha mkubwa ambaye inaonyesha kweli Simba sasa wamepania kufanya makubwa kama mambo yao yatakwenda kwa mpangilio sahihi.

Lechantre ni mmoja wa makocha wakubwa kabisa wa Kifaransa na heshima yake kwa Bara la Afrika ni kubwa kwa kuwa tayari amewahi kubeba Kombe la Mataifa Afrika.

Katika mahojiano mafupi , Lechantre alisema Afrika ni kama nyumbani kwake, si mgeni ingawa bado si mwenyeji sana kwa Afrika Mashariki.

“Nimewahi kufika Afrika Mashariki, nakumbuka nilikuwa Uganda kwa shughuli kadhaa, lakini kwa Tanzania hii ni mara ya kwanza ndiyo maana mambo mengi kwangu ni mapya.

“Lakini najua vitu vingi vya Afrika vinafanana, hivyo sina hofu hata kidogo ninajua mambo yatakwenda vizuri,” anasema Lechantre akisisitiza asingependa kuzungumza sana hadi atakapoingia mkataba na Simba.

Lechantre anaongeza: “Kuhusu Simba ni jambo jipya ingawa nina rekodi kadhaa kuwa moja ya timu imewahi kufanya vizuri katika soka Afrika. Imewahi kushinda mechi muhimu dhidi ya timu bora za Afrika Kaskazini. Haya yote yanaweza kuwa mwanzo na lazima nianze kazi kujua kila kitu.”

Wakati Lechantre anasema hivyo; msaidizi wake ni Aimen Mohamed Habibi raia wa Morocco ambaye amekuwa akifanya kazi na kocha huyo kwa zaidi ya miaka nane na yeye ndiye aliyeomba kufanya kazi na kocha huyo alisema:

“Tanzania nimekuwa nikiisikia, mimi ni mara yangu ya kwanza kabisa. Hivyo tutajua itakavyokuwa,” anasema akionekana kujiamini.

Baadaye Habibi anapata nafasi ya kujadiliana mambo mawili matatu na hampioni naC anashangazwa na namna gazeti hilo lilivyo fiti kuhusiana na soka la nchini kwake Tunisia hasa kuhusu klabu kama Esperance na Club African ambayo aliwahi kufanya kazi akiwa na Lechantre.

Kuwepo kwa Habibi, maana yake Simba kwa mara ya kwanza itakuwa na makocha wasaidizi wawili kwa kuwa kocha msaidizi mwingine ni Masoud Djuma raia wa Burundi. Kwa upande wa raia huyo wa Morocco ni mtaalamu wa masuala ya fiziki.

Maana yake kazi yake kubwa itakuwa ni kuhakikisha wachezaji wanakuwa fiti hasa kuisaidia timu na pia kusaidia kuepuka majeraha.

Lechantre ni kocha mkubwa na aliwahi kuwa mchezaji nyota katika miaka ya 1970, ambako alizichezea klabu kubwa za Ligi Kuu Ufaransa sasa inajulikana kama Ligue 1.

Lechantre alikipiga katika timu kama Lille OSC ambayo aliifungia mabao nane katika mechi 33 na pia akakipiga katika kikosi cha FC Sochaux akifikisha jumla ya mechi 211, akifunga mabao 41.

Pia amewahi kuichezea AS Monaco na Olympic Marseille, moja ya timu kubwa kabisa za Ufaransa na barani Ulaya na rasmi akaanza kazi ya ukocha mwaka 1987 akiifundisha Paris FC na baadaye AS Le Perreux.

Mwaka 1999, ndiyo rasmi alitua Afrika akianza kuifundisha timu ya taifa ya Cameroon ambayo ndiyo ilikuwa inatengeneza kizazi kipya cha wachezaji kama Rigobert Song, Samuel Eto’o, Patrick Mboma akiwa amejulikana kiasi lakini pia alimuita Marc Vivien Foe ambaye sasa ni marehemu.

Akiwa na timu hiyo aliiwezesha mwaka uliofuata tu, yaani 2000 kubeba ubingwa wa Kombe la Mataifa Afrika. Baada ya kazi hiyo nzuri Lechantre alipata ofa kubwa kwenda kufanya kazi ya kuinoa timu ya taifa ya Qatar aliyoifikisha katika fainali ya Kombe la Ghuba mwaka 2002.

Lechantre aliamua kurejea katika ngazi ya klabu na kuinoa Al Ahili SC ya Saudi Arabia, moja ya timu kubwa kabisa za nchini humo na alikaa nusu msimu kabla ya kurejea tena Qatar ambako alichukuliwa na Al Sailiya, moja ya klabu kubwa zaidi nchini humo.

Mfaransa huyo aliamua kurejea tena Afrika mwaka 2004 na kuinoa timu ya taifa ya Mali kwa mwaka mmoja na 2005, akarudi tena Qatar na kuajiriwa na timu ya mmoja wa mabilionea nchini humo ya Al Rayyan SC. Nako alikaa msimu mmoja tu kabla ya kufangasha virago vyake na kwenda Maghreb of Fez ya Morocco na 2008 akafunga safari na kuhamia nchi ya jirani ya Tunisia.

Akiwa Tunisia, Lechantre aliinoa klabu maarufu yenye mashabiki wakorofi ya Club African na hii ilikuwa kwa msimu mmoja kabla ya kutua katika klabu nyingine kubwa nchini humo ya Sfaxien Sports ambayo angalau alidumu hadi 2012 kabla ya kurejea tena barani Asia katika nchi ya Qatar na kuajiriwa na Al Arab alikojenga jina kubwa.

Huko hakudumu, aliamua kurejea Afrika na Aprili 27, 2012, aliajiriwa kama Kocha Mkuu wa Senegal lakini mwisho hakuanza hata kazi kwani baada ya wiki mbili, aliona walishindwa kutimiza matakwa yake “akachimba zake”.

Baada ya kukaa kwa miaka kadhaa, Lechantre  alirudi tena katika kazi yake ya ukocha na kwenda kuinoa Al Ittihad Tripoli ya Libya ambayo wamiliki wake ni mtoto wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Muammar Gadaffi, lakini mambo yalivyokwenda vibaya, akaondoka kwenda kuinoa timu ya taifa ya Congo yenye mji mkuu wa Brazzaville na hii ndiyo timu yake ya mwisho mwaka 2016.

Lechantre amewahi kutwaa tuzo kadhaa zikiwemo zile kubwa kama ile aliyokuwa kocha bora barani Afrika mwaka 2000-2001 na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ndilo lililomtangaza na Januari 2002 alitangazwa kuwa Kocha Bora Barani Asia kupitia Shirikisho la Soka Asia (AFC).

Amewahi kuifikisha Sfaxien ya Tunisia katika fainali ya Kombe la Caf mwaka 2010, pia ili kuonyesha kweli analijua soka la bara la Afrika.


Kwa muonekano wa kwanza, Lechantre ni mtu makini na kazi yake na anaonekana ni anayependa subira na mwepesi kuyasoma mazingira kwani msisitizo wake ilikuwa ni kwenda kuiona Simba ikiivaa Singida United hiyo jana ili ajue uchezaji wa soka la Tanzania, kikosi chake kilivyo na hata hali ya mashabiki na mwenendo mzima.

No comments:

Post a Comment