Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole ametumia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook kujibu moja kwa moja maswali aliyoulizwa na wananchi.
Kupitia mtandao huo jana, Polepole alieleza mafanikio ya CCM yaliyopatikana kwa mwaka 2017.
Katika kipindi hicho kilichoanza saa 12:00 jioni, Polepole alikuwa akisoma maswali anayoulizwa na kuyajibu, huku akiviponda vyama vya upinzani kutokana na madai kuwa wanaohamia chama hicho wanahongwa na kuliingiza Taifa gharama za uchaguzi.
Akizungumzia mafanikio ya CCM, alisema yanatokana na mabadiliko makubwa ya muundo wake kwa kupunguza idadi ya vikao na wajumbe wa ngazi zote.
Katika mabadiliko hayo, wajumbe wa Halmashauri Kuu wamepunguzwa kutoka 388 hadi 158. Pia kikao hicho kimepunguza idadi ya wajumbe wa Kamati Kuu kutoka 34 hadi 24.
“Alihama Nyalandu (Lazaro-aliyekuwa mbunge wa CCM- Singida Kaskazini) kwenda upinzani wakasifia kuwa demokrasia nzito, nzuri tusimseme ana haki na tuheshimu mawazo yake lakini Dk Mollel (Godwin-aliyekuwa mbunge wa Chadema -Siha) kaondoa kurudi CCM wanasema ni gharama ya uchaguzi,” alisema.
Alisema Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa walihama CCM na kujiunga na Chadema lakini hawakulalamika
“Kwa kazi nzuri ambayo Rais John Magufuli anafanya sijui kama atabaki mtu, Dodoma watu wamehamia CCM, huko Tarime chama kinaitwa ACT viongozi wake wote wamehamia chama tawala, mpaka tukaanza kujiuliza majengo yao itakuwaje,” alisema.
Alisema hivi sasa chama hicho kina orodha ya makada wa vyama mbalimbali wanaowaelewa.
“Wanatuelewa maana wanaoongoza kupiga vita ufisadi ni CCM, kama ulisikia mafisadi hawashikwi, CCM ndio inawashika. wanaoongoza kutoa elimu bure ni CCM na Serikali yake. Sasa huko upinzani mnafanya nini. upinzani una kazi moja tu kukosoa,” alisema.
No comments:
Post a Comment