Pages

Thursday, December 28, 2017

Rais Magufuli aipa meno kamati ya kuhakiki mali za CCM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 28 Desemba, 2017 amekutana kwa mara ya kwanza na kamati maalum aliyoiunda kwa lengo la kuhakiki mali za chama hicho, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Kamati hiyo aliitangazwa tarehe 20 Desemba, 2017 Mkoani Dodoma na inaongozwa na Dkt. Bashir Ally.

Katika Mazungumzo hayo Mhe. Rais Magufuli amewataka wajumbe wa kamati hiyo kufuatilia na kuhakiki mali zote za chama, kumhoji mtu yeyote ambaye atahitajika kutoa taarifa juu mali za chama na kubaini thamani ya mali, mahali zilipo, makusanyo ya mapato na wanaozishikilia ama kutumia mali hizo.

Mhe. Rais Magufuli pia ametoa wito kwa wanachama wa CCM na wananchi wengine kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zote zinazohusu mali za chama kwa kamati hiyo, na watakaoitwa kuhojiwa waitikie wito huo.

“Nataka mali za chama zikinufaishe chama, nataka mkamhoji mtu yeyote, awe kiongozi, awe mwanachama, awe mfanyabiashara, mtu yeyote. Mkazihakiki mali zote ili chama kipate haki yake” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Akizungumza kwa niaba ya kamati hiyo, Dkt. Bashiru Ally amesema kamati imeanza kazi rasmi na ametoa wito kwa wanachama, wananchi na wote wanaozitumia mali za chama kutoa ushirikiano watakapoitwa kuhojiwa.

“Tumezungumza na Mwenyekiti kwa karibu saa mbili, katueleza matarajio yake, sababu za kuunda tume hii, kazi zake na faida zake kwa chama na kwa nchi, kwa hiyo ametukabidhi vitendea kazi na taarifa mbalimbali na ametueleza kazi yetu ni kuhakiki mali zote za chama kwa kushirikiana na wanachama na wale wanaoshirikiana na chama kuzitumia hizo mali kama vile wapangaji, wasimamizi, nakadhalika” amesema Dkt. Bashiru Ally.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
28 Desemba, 2017

No comments:

Post a Comment