Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo
tarehe 09 Januari, 2018 amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu
Mstaafu Mhe. Edward Ngoyai Lowassa, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Baada ya mazungumzo hayo Mhe. Edward Ngoyai Lowassa amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya na ametaja baadhi ya maeneo ambayo kazi kubwa imefanyika kuwa ni kutoa elimu bila malipo, ujenzi wa mradi wa uzalishaji wa umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge), ujenzi wa viwanda na ujenzi wa reli kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) ambavyo vinazalisha ajira nyingi kwa Watanzania.
“Nimepata
faraja sana kuja hapa Ikulu kuonana na Mhe. Rais, tumezungumza nae na
nimempongeza kwa kazi nzuri anayoifanya, lazima tukiri anafanya kazi
nzuri na anahitaji kutiwa moyo.
“Moja
kubwa ambalo ni la msingi sana ni la kujenga ajira, katika kuanza
ujenzi wa reli ya kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro hapo anajenga
ajira, na kwenye nchi yoyote inayoendelea suala muhimu ni kujenga ajira,
Stiegler;s Gorge ni kujenga ajira na mingine ya aina hiyo, lazima
kuwepo na kipaumbele cha kusema kwamba tunajenga ajira, jingine ni la
elimu, ni muhimu sana, hauwezi kuacha elimu katika mambo yako
unayofanya, hili nalo lazima lisemwe vya kutosha, kwa kweli nakushukuru
Mhe. Rais, you made my day” amesema Mhe. Lowassa.
Kwa
upande wake Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Edward Ngoyai Lowassa
kwa kutambua kazi kubwa inayofanywa na Serikali na amesema Mhe. Lowassa
ni mmoja wa viongozi ambaye kwa wakati wake ametoa mchango wake katika
nchi.
Mhe.
Rais Magufuli ameongeza kuwa Mhe. Lowassa ni mwanasiasa mzuri kwani
hata wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita ambao naye aligombea
kiti cha Urais, hakuwahi kumtukana.
“Mhe.
Lowassa ameniomba mara nyingi nikutane nae, na leo nimekutana nae,
tumezungumza mambo mengi, ameniambia ya kwake na mimi nimemwambia ya
kwangu, kwa ujumla Mhe. Lowassa ni mwanasiasa mzuri na tuendelee
kuwaenzi wazee hawa ambao kwa nyakati fulani walifanya mambo mazuri, na
mimi napenda kumpongeza Mhe. Lowassa ambaye kama alivyosema hapa kuwa
tumefanya mambo mazuri mengi.
“Ametaja
miradi mbalimbali tunayotekeleza, ametaja mradi wa Stiegler’s Gorge
utakaogharimu zaidi ya Shilingi Trilioni 7, amezungumzia juu ya elimu
bure, amezungumzia juu ya maji ambayo kwa bahati nzuri yeye alikuwa
Waziri wa Maji na anafahamu sasa tumefikia wapi, amezungumza juu ya
umeme tulivyosambaza katika vijiji mbalimbali, elimu bure, huduma za
hospitali na mengine” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
09 Januari, 2018
No comments:
Post a Comment