Mbunge wa jimbo la Msalala Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga Ezekiel Magolyo Maige ameibuka na kusema kuwa yeye si wa kulinganishwa na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda.
Maige alitoa kauli hiyo Januari 8 mwaka 2018 katika mkutano wa hadhara kwenye ziara yake kijiji cha Sungamile kata ya Mwalugulu wilayani Kahama mkoani Shinyanga.
Hoja ya Maige imekuja mara baada ya mwanchi mmoja aliyejulikana kwa jina la Jumanne Moshi kuibua hoja ya kuusifu utendaji kazi wa mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda huku akiwataka viongozi wengine akiwemo mbunge kufuata utendaji huo.
"Namsifu sana mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam kwa sababu anafanya ubunifu,anapoona hakuna pesa anachangisha yeye mwenyewe kwa matajiri ili kutekeleza miradi"Alisema mwananchi huyo.
Akijibu hoja hiyo mbunge wa jimbo la Msalala ambaye pia aliwahi kuwa waziri wa Maliasili na utalii Ezekiel Magolyo Maige alisema kuwa Makonda ni mwanafunzi kwake.
"Jumanne Moshi anatoa mfano anasema viongozi tuige utendaji kazi kwa Makonda nataka niseme tu kwamba Makonda ni Mwanafunzi wangu ameiga kwangu.Mimi huyu huyu nimejenga mabweni hapo Isaka ya Zaidi Milioni 200 bila kuchanga hata shilingi na wananchi,Mimi huyu huyu nimeweza kujenga Mabweni Busangi ya zaidi ya shilingi milioni 130 bila wananchi kuchanga,Mimi huyu huyu hivi sasa tumepata pesa za TARURA zaidi ya Shilingi Milioni 300 katika ujenzi wa barabara kutoka Mwankima,Mwakuhenga ,na Ntobo.Jimbo la Msalala limepata pesa nje ya bajeti zaidi ya Tsh.milioni 400.
Tofauti mimi na Makonda mimi kama msomi niliyebobea situmii vyombo vya habari .Kwa kifupi sana Makonda ni mwanafunzi wangu na ninaendelea kumfundisha ili aweze kubobea katika eneo lake".
Alisema mbunge huyo.
Ziara ya Maige inaendelea katika maeneo mbalimbali katika eneo la Msalala kwa lengo la kusalimia na kuhamasiha shughuli mbalimbali za Maendeleo.
No comments:
Post a Comment