Naibu
Waziri wa Madini, Doto Mashaka Biteko ambaye ameapishwa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Naibu
Waziri katika Wizara ya Madini tarehe 8 Januari, 2018 ameanza kazi rasmi
kwa kufanya kikao na Viongozi na Watumishi wa Wizara husika.
Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Wizara jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo na Katibu Mkuu, Profesa Simon Msanjila.
Akizungumza
katika kikao hicho, Naibu Waziri huyo alieleza kuhusu umuhimu wa kuwepo
kwa ushirikiano kati ya viongozi na watumishi wa Wizara ili kwa pamoja
wasimamie ipasavyo Rasilimali Madini na kuhakikisha kuwa inafaidisha
Taifa.
“Ili
kutimiza malengo ya Rais wetu ya kuhakikisha kuwa Rasimali Madini
inaendelezwa ipasavyo, hatuna budi kushirikiana na kushikamana ili kuwe
na umoja utakaoleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu kwani sisi
sote ni watumishi wa watanzania,” alisema Biteko.
Kwa
upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amesema kuwa
Uteuzi wa Naibu Waziri wa Pili katika Wizara ya Madini unaonesha namna
Rais John Magufuli anavyoichukulia kwa umuhimu wa pekee Sekta ya Madini
ambayo ni muhimu katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
“Tutashirikiana
kwa pamoja na watumishi wa Wizara ili kuweza kusukuma gurudumu la
maendeleo ya Taifa mbele zaidi,” alisema Nyongo.
Kwa
upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila
alisema kuwa viongozi hao na watumishi kwa pamoja watafanikisha
mategemeo na malengo ya Rais John Magufuli ya kuhakikisha kuwa Rasimali
Madini inalinufaisha Taifa.
Aidha
alitumia fursa hiyo kuwaeleza watumishi kuhusu uamuzi wa Rais John
Magufuli wa kutengua uteuzi wa Kamishna wa Madini, Mhandisi Benjamin
Mchwampaka na kumteua Profesa Shukrani Elisha Manya kuwa Kamishna wa
Madini na pia kukaimu nafasi ya Mtendaji Mkuu wa Kamisheni ya Madini na
hivyo kuwaasa watumishi kumpa ushirikiano Kamishna huyo mpya.
No comments:
Post a Comment