Na. WFM
Benki
zote nchini Tanzania na Kampuni za Mawasiliano zinatakiwa kuwa
zimejiunga na mfumo wa wa Kielektroniki wa kukusanya mapato kupitia
kituo cha Data kilichopo Kijitonyama Jijini Dar es Salaam ifikapo
Januari 31, 2018 kinyume na hapo Serikali itanyang’anya Leseni za
uendeshaji wa shughuli zao hapa nchini.
Agizo
hilo limetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor
Mpango (Mb) alipokutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Benki
Jijini Dar es Salaam.
Amesema
kuwa mwaka 2017 zilitungwa Kanuni za Sheria za utawala wa Kodi ambao
ulizitaka Benki na Kampuni za Simu kuwa zimejiunga na Mfumo wa
kielektroniki wa kukusanya kodi kati ya Juni, 2017 hadi Desemba 31, 2017
na mpaka sasa ni Benki 27 tu ambazo zimetekeleza hatua hiyo ya
Kisheria.
‘Nimekutana
na Benki takribani 20 ili kuwasikiliza ni kwanini hawajatekeleza
matakwa ya sheria na katika mjadala huo nimebaini sababu kadhaa
zilizosababisha baadhi ya Benki kuchelewa kuchukua maamuzi, miongoni mwa
sababu hizo ni hofu kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania ambayo inaweza kuona
miamala na hivyo kuweza kusababisha wizi wa kimtandao” alieleza Dkt.
Mpango.
Sababu
nyingine ni pamoja na Matakwa hayo kuja ghafla hivyo kuhitaji fedha za
dharula na Benki kubwa kama City Bank kuwa na mtandao mkubwa Kimataifa
wa nchi takribani 100 hivyo kuwalazimu kuwasiliana na Makao Makuu ya
Benki hiyo kabla ya kufanya Maamuzi.
Hata
hivyo kwa kuwa tayari wamevunja sheria iliyowataka kutekeleza agizo la
Serikali kufikia Desemba 31, 2017, Waziri Mpango amemuagiza Kamishna
Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Charles Kichere kuwachukulia hatua
za kisheria ikiwemo faini katika kipindi walichoshindwa kutekeleza
sheria.
Dkt.
Mpango amezipongeza Benki zilizotekeleza Sheria ndani ya muda uliowekwa
kuwa ni pamoja na Exim Bank, Benki ya NMB, Benki ya Posta, Amana Benki,
CRDB, China Comnercial Bank, Stanbic na Akiba Commecial Bank na
nyingine.
Benki
ambazo zipo katika hatua nzuri ni pamoja na I&M, DCB, DTB, Mkombozi
Bank, Maendeleo Bank wakati Benki ambazo hazijapiga hatua kuwa ni
pamoja na Bank of Africa, Yetu Microfinance Bank, Barclays na Mwanga
Rural community Bank.
Kwa
upande wa Mikopo Chechefu katika Benki, Waziri Mpango ameeleza kuwa
hali haikuwa nzuri kwa mwaka 2017 kwa kuwa Mikopo Chechefu ilifikia
asilimia 12 ya mikopo yote ya Sekta ya Benki ambapo kwa sasa Wadau wa
Benki wameona kuna hatua nzuri katika eneo hilo hivyo kufanya Sekta hiyo
kuimarika.
Ameeleza
kuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iko imara na Sekta ya Benki kwa sasa
ina ukwasi wa kutosha na si kweli kama mikopo chechefu inaiangusha sekta
hiyo.
Amezitaka
Benki nchini kuwa na mfumo mzuri unaofuata taratibu za mikopo ili
kutatua tatizo hilo kwa kukopesha watu wenye vigezo na pia Mahakama
imetakiwa kuheshimu dhamana za awali zilizowekwa na wakopaji kwa kuwa
kuna wanaokubaliwa dhamana zao na baadaye Mahakama inasema dhamana hizo
hazipo halali jambo linaloongeza uwepo wa mikopo hiyo chechefu.
No comments:
Post a Comment