Pages

Monday, January 8, 2018

Serikali yaitaka Stamigold ijiendeshe kibiashara


Serikali imetoa siku 14 kwa kampuni ya Stamigold, inayomiliki Mgodi wa Dhahabu uliopo Biharamulo mkoani Kagera, kuandaa mpango mkakati wa kibiashara, utakaobainisha namna itakavyojiendesha pasipo kuitegemea Serikali.

Agizo hilo lilitolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila alipotembelea Mgodi huo na kuzungumza na Menejimenti pamoja na wafanyakazi wake.

Profesa Msanjila alisema kuwa lengo la Serikali kupitia Wizara ya Madini, ni kuona Kampuni tanzu hiyo ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), inajiendesha kibiashara na kiushindani ili ipate faida stahiki na kulinufaisha Taifa kama ilivyo dhamira ya kuanzishwa kwake, na siyo vinginevyo.

“Menejimenti ya Kampuni, Bodi pamoja na Menejimenti ya STAMICO, nawapa hadi tarehe 21 mwezi huu, kila upande uwe umewasilisha mapendekezo ya kimkakati yanayobainisha namna gani Stamigold itaweza kusimama yenyewe na kujiendesha kiushindani kama zilivyo kampuni nyingine za kibiashara. Kwa upande wetu, Kamishna wa Madini na mimi Katibu Mkuu pia tutakuja na mapendekezo yetu.” alisema Profesa Msanjila.

Akifafanua zaidi, Katibu Mkuu alisema Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika kampuni ya Stamigold hivyo haitakubali kuona mgodi huo unaendeshwa kwa hasara. “Kila mtu awajibike kwenye eneo lake,” alisisitiza.

Alisema, pamoja na kuwa Stamigold ni kampuni ya Serikali lakini imesajiliwa na Taasisi inayotoa leseni za biashara ya Brela, hivyo inapaswa kujiendesha kama kampuni nyingine za kibiashara. 
“Kampuni ya serikali ambayo haifanyi biashara haiendi kujiandikisha Brela. Ninyi mnafanya biashara hivyo lazima mfanye kazi kibiashara.”

Aidha, Profesa Msanjila aliutaka uongozi wa kampuni kuhakikisha unaweka wazi taarifa zote za mapato na matumizi kwa wafanyakazi wote ili waelewe wanazalisha kiasi gani, wanapata faida kiasi gani, matumizi ni kiasi gani na kama kuna hasara ibainishwe wazi.

Alifafanua kuwa utaratibu wa kuweka wazi mapato na matumizi kwa wafanyakazi wote utaondoa manung’uniko kwani utaratibu wa kibiashara unamtaka mwajiri amlipe mfanyakazi kulingana na mapato. 
“Huwezi kumlipa mtu mshahara hata pale ambapo hazalishi. Hii siyo sawa kibiashara maana lazima utapata hasara. Huu ndiyo ukweli ndugu zangu. Tubadilike. Hakuna hela ya kuchezea.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Mhandisi John Nayopa alimhakikishia Katibu Mkuu kuwa maagizo yote aliyoyatoa yatatekelezwa ndani ya muda alioelekeza. 
Aidha, aliwataka wafanyakazi wa Stamigold kutoa ushirikiano kwa kutoa maoni na ushauri wao wakati wa kuandaa mpango mkakati huo utakaoiwezesha Kampuni kujiendesha kibiashara.

Katika ziara hiyo, Katibu Mkuu aliambatana na viongozi wengine wa Wizara akiwemo Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimaliwatu, Miriam Mbaga, Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Ziwa Viktoria Magharibi, Mhandisi Yahaya Samamba, Kaimu Afisa Madini wa Mkoa wa Kagera, Paschal Bundala na Mhandisi Migodi kutoka wizarani, Kungulu Kasongi.

No comments:

Post a Comment