Pages

Tuesday, December 26, 2017

OMOG SAWA, LAKINI MADUDU YA VIONGOZI, WACHEZAJI BADO NI MAGUGU SIMBA



Na Saleh Ally
KOCHA Joseph amefutwa kazi katika kikosi cha Simba na uongozi wa klabu hiyo ukaendeleza uungwana wake wa kusema wamekubaliana kuvunja mkataba, hii haina tofauti na ile hali aliyoondoka nayo Kocha Msaidizi, Jackson Mayanja raia wa Uganda ambaye ilielezwa “ameomba”.

Kuondoka kwa Omog ni baada ya Simba kulazwa mabao 4-3 kupitia mikwaju ya penalti dhidi ya timu ya Green Worriers inayoshiriki Ligi Daraja la Pili. Kipigo pekee si jambo linalowaumiza Simba, badala yake ni maumivu ya kuvuliwa ubingwa.

Huenda hata kuondoka kwa Kocha Joseph Omog inawezekana ikawa si maumivu ya Wanasimba wote, ni maumivu ya mwanachama maarufu zaidi wa Simba, Mohamed Dewji ambaye aliandika mtandaoni kuhusiana na msimamo wake baada ya Simba kuvuliwa ubingwa akisema hana nguvu kwa kuwa ni mwanachama wa kawaida na kama ni mawazo, basi anamuomba Omog apumzike.

Haikupita zaidi ya saa moja, Omog tayari alikuwa katika matatizo na saa moja baadaye akaondolewa na kuondoka kwake kumebaki kukiwagawa Wanasimba wengi, wapo wanaokubali na wanaopinga na hili limekuwa ni jambo la kawaida.

Lengo la kumuondoa Omog ni kufanya vizuri, kocha huyo anaondoka akiwa na rekodi nyingi ndani ya misimu miwili na ushee ndani ya kikosi hicho. Kwani baada ya miaka minne ya kusota ndiye aliyeirudisha katika michuano ya kimataifa baada ya kutwaa Kombe la Shirikisho ambalo leo limeng’oa Simba.



Achana na rekodi yake akiwa Azam FC kuchukua ubingwa bila ya kufungwa hata mechi moja, aliiongoza Simba mechi tisa bila kuruhusu hata bao moja na akashika nafasi ya pili nyuma ya mabingwa Yanga akiwa nao pointi sawa, wao wakichukua ubingwa kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Lakini hata wakati anaondoka kikosi cha Simba kipo kileleni, hivyo unaweza kusema ni kocha aliyetupiwa virago akiwa na kumbukumbu nzuri na alichokuwa anakifanya na hakuna ubishi, siku chache zijazo, Simba “watamkumbuka”.

Unaweza kujiuliza maswali mengi, kwamba kufukuzwa kwake Simba ndiyo muarobaini sahihi na utaisaidia klabu hiyo. Nafikiri kuna mengi ya kujifunza nikianza na yafuatayo.

Mo Dewji:
Mo Dewji ndiye atakuwa mwekezaji mkuu hapo baadaye kwa kuwa mchakato umepita na yeye ameshinda zabuni. Hakika ameonyesha mfumo wa wafanyabiashara walivyo, inapobidi anachukua hatua badala ya kusubiri.

Kuna haja pia ya kuwa na washauri kwa kuwa ikiendelea hivyo akawa anachukua uamuzi wake kupitia maumivu ya moyo wake, wakati mwingine haitakuwa sahihi. Badala yake, linapotokea tatizo vizuri kuangalia mambo kadhaa kabla ya kuchukua uamuzi.

Viongozi:
Leo hakuna kiongozi anayewajibika, lakini viongozi wakiwemo wale wa kamati ya usajili wanajua wapi wamemkwamisha Omog au kumsaidia. Ukweli kuna sehemu walikuwa na matakwa yao binafsi na tunajua sote ndani ya kamati kuna wachezaji huletwa na watu na watu wangefurahi kuona waliowaleta wanacheza.

Kamati ya Usajili ya Simba si miungu, wao pia wanakosea na hakuna anayeadhibiwa. Wanaitia klabu hasara na hakuna anayehojiwa, lakini adhabu ya Omog inaonyesha makosa yao pia na wanahusika.

Kusajiliwa kwa baadhi ya wachezaji au kuachwa hata kama Omog hakutaka nalo lilikuwa kosa. Alitoa mapendekezo yake ya mshambuliaji, kipa na beki. 

Hayakutekelezwa yote, amesajiliwa mchezaji asiyemjua, hakupewa hata video, jambo ambalo kitalaamu nalo si zuri. Mnajua mlimkwamisha wapi, basi vizuri mjipange ili ajaye msimuangushe na mwisho aadhibiwe yeye.



Wachezaji:
Kama alivyofanya Mo, nafikiri ingekuwa inawezekana basi Simba ingechukua hatua kwa wachezaji au kuna haja ya kurekebisha mikataba yao kuwa kama kuna uzembe kazini adhabu inapita.

Mechi nyingi za Simba angalia wachezaji walivyo mastaa, ajabu walio Barcelona na Real Madrid wanajituma kwa juhudi kubwa kuliko walio Simba ambalo ni jambo la kusikitisha sana.

Simba iliyoshindwa kuifunga Green Worriers katika dakika 90, wachezaji wanakwenda kupiga penalti utafikiri mpira ulishaingia wavuni, tena hawaonyeshi wamelenga kushinda. Wamelegea, hakuna malengo kwenye macho wala miili yao. Siku ile wachezaji wa Green Worriers ndiyo waliopaswa kuitwa wachezaji wa Simba na Simba wawe Green Worriers.



Omog angewaadhibu, uongozi na mashabiki ungepiga kelele. Kwa kuwa wamejenga mapenzi nao na wamewafanya washindwe kuheshimu anayewaongoza na wanataka kuheshimu wao juu yake.

Wachezaji wengi wa Simba wanaamini Simba imebahatika “kuchezewa” na wao, hawajui wamekuwa na bahati kubwa kuitumikia Simba!

Mashabiki:
Kundi la mwisho lenye sapoti kwa timu lakini linaweza kuwa sumu hasa kama uongozi si imara. Walilia na Mkude arudishwe kucheza wakati kocha alimuona hana msaada, Mkude alirudi baada ya kushindwa kuonyesha juhudi akaonyesha baada ya kuona ameombewa nafasi, jiulize awali kwa nini hakufanya hivyo?

Wachezaji hawajitambui kwa kuwa wanajua wana watetezi ambao ni mashabiki. Tangu Mkude amerudi, mara ngapi Simba imetoka sare au imefungwa? Mara ngapi ameiangusha? Jibu litakuwa “ni mambo ya soka”. Lakini kwa nini kwa Omog haikuwa “mambo ya soka?”

Kuna sababu ya kujifunza, mashabiki wajadili na kushangilia kazi wamuachie kocha na atakayekuja wampe nafasi ili wale waliovimba vichwa awanyooshe na kazi iwe ya uhakika.


Kila la kheri Omog, ulistahili kwenda lakini waliokuangusha umewaacha wanaendelea “kula bata” na sasa watakuwa na muda wa kujituma kuwasahaulisha Simba kabla ya kuendelea na “kama kawaida” hapo baadaye.

No comments:

Post a Comment